Washukiwa wa sakata ya Rio wafikishwa mahakamani

Washukiwa wa sakata ya Rio wafikishwa mahakamani

Aliyekuwa waziri wa michezo Hassan Wario na aliyekuwa rais wa kamati ya kitaifa ya Olympiki Kipchoge Keino wamepewa hadi siku ya Alhamisi kujisalimisha kwa polisi kuhusiana na sakata ya fedha za michezo ya Olympiki ya mwaka wa 2016.

Wawili hao walikuwa miongoni mwa maafisa wanne waliokosa kufika mahakamani kujibu mashtaka yanayohusiana na utumizi mbaya wa pesa za umma.

Aliyekuwa katibu katika wizara ya michezo Richard Ekai na waliokuwa maafisa wa shirikisho la Olimpiki NOCK Stephen Soi na Francis Kinyili walikanusha mashtaka dhidi yao kuhusiana na sakata ya million 55 ya michezo ya olimpiki iliyofanyika Rio, Brazil.

Kiongozi wa mashtaka aliidhinisha kushtakiwa kwa maafisa hao akisema kuna ushahidi wa kutosha.

Wameshtakiwa kwa kuhusika katika ufujaji wa shilingi milioni 22.5, shilingi milioni 16.8 za tiketi za ndege ambazo hazikutumika mbali na shilingi milioni 6.5 zilizotumika na watu ambao hawakustahili wala kuidhinishwa.

Ekai na washtakiwa wenzake wawili waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni mbili au milioni moja pesa taslim.

Wario, Keino na waliokuwa maafisa wa NOCK Kiptanui Arap Soi na Patrick Kimanthi walikosa kufika mahakamani leo na wanatakiwa kufika katika makao ya DCI siku ya Alhamisi kabla ya kufika kortini Ijumaa.

Tags:

Rio scandal

Leave a Comment

Comments

No comments yet.

latest stories