JAMILA’S MEMO: A letter to President William Ruto

Jamila Mohamed
By Jamila Mohamed September 16, 2022 12:05 (EAT)
JAMILA’S MEMO: A letter to President William Ruto
Vocalize Pre-Player Loader

Audio By Vocalize

Hujambo Mheshimiwa Rais William Ruto. Ni siku mbili sasa tangu uapishwe rasmi kama rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya. Hafla ya kuapishwa kwako ilikuwa na mbwembwe na sherehe, lakini pia ilikuwa na matumaini makubwa miongoni mwa Wakenya wengi; matumaini kuwa maisha yao yatakuwa bora zaidi, matumaini kwamba ahadi ulizotoa za kuimarisha maisha ya mwananchi na kumpunguzia changamoto za kila siku zitatimia.

Tayari umewaapisha majaji sita wa mahakama, na kutimiza mojawapo ya ahadi ulizotoa, na kuwapa wananchi matumaini ya kupata haki wanapoelekea mahakamani. Kuimarisha huduma za idara ya polisi kwa kuweka mikononi mwa inspekta jenerali wa polisi mkoba wa kuendesha shughuli za idara hiyo; matumaini kuwa wananchi waatakapokimbia kwa polisi kutafuta usaidizi, wataupata kwa haraka.

Bei ya mbolea, na pembejeo za kilimo ambazo wakulima wanaweza kumudu, itakuwa afueni kwa wakulima na Wakenya wote kwa ujumla. Gharama ya maisha iko juu, wengi wanashindwa hata kupata chakula cha kulisha familia zao; utakuwa umewaondolea mzigo mkubwa iwapo bei ya chakula itakuwa nafuu.

Masomo kwa watoto na uwezo wa wazazi kugharamia masomo hayo ni jambo linguine. Hali ngumu inawakumba wazazi wengi ambao wanahangaika kila mara shule zinapofungwa kwani tayari wanafikiria karo itatoka wapi shule zitakapofunguliwa, na ahadi za elimu bora kuliko bora elimu, miundo mbinu shuleni, walimu wa kutosha, nafasi shuleni na mtaala unaofaa.

Ahadi za ajira kwa vijana na nafasi zaidi kwao kuendelea mbele katika maisha yao; wengi wanahangaika usiku na mchana wakitafuta nafasi yoyote, popote pale angalau wapate cha kuweka mfukoni. Na sio kwa sababu hawajasoma, la, wengi wao wamehitimu ila stakabadhi hizo sasa zimekuwa mzigo wa kubebwa hapa na pale kutafuta nafasi za kazi. Vijana hawa wanakutazama wakisubiri kutimizwa kwa ahadi yao.

Wanaoendesha biashara ndogo ndogo na wanaohitaji kupewa usaidizi kuanzisha biashara pia wako hapo pembeni. Iwapo watu wengi zaidi watapata mazingira bora ya biashara na usaidizi wa kuanza na kuendelea na biashara zao, idadi ya wale wanaosubiri kuajiriwa itapungua; wataweza kujitegemea na kusaidia familia zao.

Na kwa wanawake je? Wanasubiri nafasi uongozini, ni furaha kubwa kushuhudia kina mama zaidi wakichaguliwa na wananchi katika nyadhifa za juu; ishara tosha kwamba wananchi wanaanza kuwa na imani na uongozi wa mama. Na bado wanawake wanasubiri ahadi kwao ya nafasi zaidi serikalini. Itakumbukwa kuwa Rais Ruto aliahidi kuwa asilimia 50 ya baraza la mawaziri litakuwa ni wanawake; mbali na hayo, juhudi za kuwasaidia kupata mazingira bora ya kufanya biashara zinasubiriwa.

Huduma bora hospitalini; kuwepo kwa madaktari, wauguzi, dawa na vifaa vya kutambua magonjwa. Wengi wanatarajia wataweza kumudu gharama inayoambatana na matibabu, wamechoshwa kuwatazama wapendwa wao wakihangaika kwa kukosa huduma bora za matibabu.

Unaona mheshimiwa rais, mahitaji ya wananchi sio mengi; chakula cha kila siku, masomo kwa watoto, nafasi za ajira, huduma bora za matibabu ni mambo muhimu kwa mwananchi wa kawaida. Safari yako ndio inaanza, sio safari rahisi, macho ya mamilioni ya Wakenya yanaelekezwa kwako na serikali utakayounda. Na bila shaka kutakuwa na panda shuka za hapa na pale, ila ukiweka kipaumbele mahitaji ya wananchi na kutimiza ahadi za kuimarisha maisha yao, utakuwa umefaulu machoni mwao.

Na mwisho kabisa Rais Ruto, huu ni wakati wa kumfikiria kila Mkenya, yule aliyekupigia kura na yule ambaye aliweka kura yake kwingine. Itakuwa bora ukiweka juhudi zaidi kuwapa mkono Wakenya ambao huenda wanaona hawamo ama hawana nafasi popote kwa sababu kiongozi wao alishindwa. Na kwamba sio wote waliokuwa nawe wakati wa kampeini watakufaa serikalini, unakumbuka rais mstaafu Moi alisema uongozi ni tofauti.

And that is my Memo!

Join the Discussion

Share your perspective with the Citizen Digital community.

Moderation applies

Sign In to Publish

No comments yet

This discussion is waiting for your voice. Be the first to share your thoughts!